Mkuu wa wilaya ya Mbogwe Mhe. Martha Mkupasi amewataka madiwani wenye vijiji vyenye walengwa wa mpango wa TASAF awamu ya tatu kuwaelimisha wanufaika wa mpango huo wa kunusuru kaya maskini kuhusu umuhimu wa kuweka akiba na kukuza uchumi wa kipato cha kaya.
Mkuu wa wilaya ameyasema hayo wakati wa kufungua kikao kazi cha waheshimiwa Madiwani, Wakuu wa Idara pamoja na Maafisa Ugani wa wilaya ya Mbogwe kilichofanyika leo tarehe 8-5-2018 katika ukumbi waHalmashauri.
Kikao hicho kimeendeshwa na wataalam kutoka TASAF makao makuu pamoja na Wataalam kutoka Halmashauri za wilaya ya Ikungi na Mbogwe, kikiwa na lengo la kuwajengea uwezo waheshimiwa Madiwani ,Wakuu wa idara na Maafisa ugani ili wawe na uelewa sahihi kuhusu uwekaji wa akiba na ukuzaji wa uchumi wa kaya.
Mpango wa TASAF awamu ya tatu umeanza rasmi Wilayani hapa ukiwa unatekeleza kipengele cha tatu cha kuondoa umaskini wa kaya kiitwacho "Kuweka akiba na kukuza uchumi wa kipato cha kaya""
Ambapo kipengele cha kwanza na cha pili yaani uhawilishaji fedha na miradi inayotoa ajira za muda vitaendelea sambasamba na kipengele hiki kipya cha tatu kinachoanza rasmi kupitia fedha wanazopata katika uhawilishaji na pia kazi wafanyazo katika miradi ya ajira za muda, wataweza kuweka akiba ili kuinua kipato cha kaya.
Pamoja na hayo muwezeshaji wa mafunzo toka TASAF makao makuu ndugu Sesil Charles Latemba amewaomba Waheshimiwa Madiwani kuwa mabalozi wazuri katika kuwaelimisha wananchi kuhusu utunzaji wa akiba,
Vile vile amewasisitizia wazingatie kuwa uundwaji wa vikundi vya kujiwekea akiba ni swala la hiari hivyo wajikite katika kuwaelimisha umuhimu wa kuwa kwenye vikundi.
Pia Bwana Latemba amewaambia Madiwani wakati akijibu swali la mmoja wa washiriki kwamba vijiji ambavyo havikuingizwa kwenye mpango, jitihada za Serikali, wadau wa maendeleo na TASAF bado zinaendelea ili hatimaye Vijiji hivyo viingizwe kwenye mpango, kwa sasa wasiwaahaidi wananchi chochote mpaka hapo itakavyoelekezwa rasmi kufanya hivyo.
Akiongea kwa niaba ya Madiwani, Diwani wa Kata ya Ilolangulu Mhe. Ndabacha Simon ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuwajali wananchi maskini, pia kuanza mchakato wa kuviongeza vijiji ambavyo havikuwa kwenye mpango wa TASAF.
Mbogwe District council ,Masumbwe-Mbogwe,Geita
Postal Address: P.O Box 1 Masumbwe
Telephone: +255734412592
Mobile: +255734412592
Email: ded@mbogwedc.go.tz
Copyright ©2016 GWF . All rights reserved.